CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimezidi kuilaumu iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuandika rasimu iliyojaa mawazo ya wajumbe wake waliotaka muundo wa serikali tatu. Lawama hizo zilitolewa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Mwembeyanga jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo uliandaliwa kwa lengo la kumpongeza Rais Jakaya
Kikwete, kwa hotuba aliyoitoa bungeni Machi 21, ambapo Kinana alisema tume hiyo
iliyokuwa chini ya kada wao Jaji Joseph Warioba, haikueleza ni makundi mangapi
yalitaka serikali tatu.
Kinana alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba walisubiri
Mwalimu Julius Nyerere afe ndipo waseme serikali tatu, kwani walikuwepo enzi
hizo.
“Muungwana angesema nani kasema nini wakati wa kuchukua
maoni, tume haijasema katika mabaraza 171 ni mangapi yalitaka serikali tatu,
ukiwauliza mara makaratasi yamepotea, hatukumbuki.
“Tusitoane meno na
macho kwa ajili ya Katiba, kwani ikishatengenezwa itawekwa kabatini na viongozi
wataendelea kula kuku, umaskini upo palepale, ufisadi upo palepale,
alichokisema Rais Jakaya Kikwete ni tahadhari tu, yapo maisha baada ya Katiba,”
alisema.
Kinana alibainisha kuwa wamepata taarifa kuwa baadhi ya
wajumbe wa Bunge Maalumu kutoka upinzani wamedhamiria kuvuruga vikao vya Bunge
ili Katiba mpya isipatikane.
Alisema wajumbe hao wanafanya hivyo baada ya kuona hawawezi
kuingiza matakwa yao, kwakuwa wingi wa wajumbe wa CCM unawatisha.
Katika hatua nyingine, Kinana alisema kuwa ziara yake ya
siku nne jijini Dar es Salaam ya kukagua miradi imeonyesha namna CCM ilivyopiga
hatua katika utekelezaji wa ilani.
Alisema kuhusiana na suala la maji alitembelea Ruvu Chini na
Juu na kubaini kuwa ifikapo mwaka 2015 asilimia 72 ya wakazi wa Dar es Salaam
watapata maji ingawa Wizara ya Maji inakabiliwa na uhaba wa fedha.
Akizungumzia masuala ya umeme, Kinana alisema anayetaka
umeme wa bei nafuu ahamie kijijini, kwani gharama za umeme mijini na vijijini
ni tofauti.
Kuhusu mji mpya wa Kigamboni, alisema kuwa watalizungumza
suala hilo ili kulipatia ufumbuzi.
“Hatujawahi kuona mji mpya unajengwa kwa kuhamisha watu,
kama serikali imeamua mbona hawakuuliza wananchi?” alihoji.
Alisema kuwa matatizo ya walimu yataendelea kutatuliwa
ikiwemo serikali kuendelea kujenga nyumba za walimu na kuwapunguzia makali ya
ugumu wa maisha.
Kawa upande wa tatizo la ajira, aliitaka serikali kutafuta
mbinu zisizo za kawaida za kutengeneza ajira nyingi zaidi ili watu wengi
waajiriwe, hasa watu wa chini kwa kutengeneza viwanda vingi.
“Watu wanaojiajiri wapewe nafasi, si mgambo kuwasumbua na
kuwadai kodi zisizo na msingi, kodi ndogondogo zinasumbua watu na kupoteza
muda,” alisema.
Kuhusiana na tatizo la wizi wa dawa hospitalini, Kinana
alisema kuwa serikali imepata suluhisho ambapo dawa zote zitaandikwa Serikali
ya Tanzania
Kinana alisema ifike mahali matatizo yanayoikabili nchi
yatatuliwe, kwani wao kazi yao ni kuisimamia serikali na kuwajibishana pale
panapokosewa.
Naye Mbunge wa Ilala, Idd Zungu, alisema Bunge halikutunga
sheria kandamizi kwa bodaboda na wafanyabiashara bali Mamlaka ya Udhibiti wa
Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra)
ndio waliotunga kanuni kandamizi

Nikweli kabisa.
JibuFutaCCM kwanini mnalia na Warioba wakati mliteua wenyewe?
JibuFuta